Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 24:4-28

Mathayo 24:4-28 BHN

Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. Maana wengi watatokea wakisema kila mmoja kwamba yeye ndiye Kristo nao watawapotosha watu wengi. Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. “Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu. Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote. “Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. “Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: ‘Kristo yuko hapa’ au ‘Yuko pale,’ msimsadiki. Maana watatokea akina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha waonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, ‘Tazameni, yuko jangwani,’ msiende huko; au, ‘Tazameni, amejificha ndani,’ msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.