Luka 11:1-13

BHN
Biblia Habari Njema

1Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.” 2Yesu akawaambia, “Mnaposali, semeni:
‘Baba!
Jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike.
3Utupe daima chakula chetu cha kila siku.
4Utusamehe dhambi zetu,
maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea;
wala usitutie katika majaribu.’”
5Kisha akawaambia, “Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: ‘Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu, 6kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.’ 7Naye, akiwa ndani angemjibu: ‘Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!’ 8Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. 9Kwa hiyo, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni mlango nanyi mtafunguliwa. 10Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye mlango hufunguliwa. 11Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki? 12Na kama akimwomba yai, je, atampa nge? 13Kama nyinyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba.”