Luka 1:67-80
Luka 1:67-80 BHN
Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu: “Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amewajia na kuwakomboa watu wake. Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. Alimwapia Abrahamu babu yetu, kwamba atatujalia sisi tukombolewe mikononi mwa maadui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atatuchomozea mwanga kutoka juu, na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.” Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.