Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 3:1-39

Maombolezo 3:1-39 BHN

Mimi ni mtu niliyepata mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake Mungu. Amenichukua akanipeleka mpaka gizani kusiko na mwanga. Amenyosha mkono wake dhidi yangu mimi tu, akanichapa tena na tena mchana kutwa. Amenichakaza ngozi na nyama, mifupa yangu ameivunja. Amenizingira na kunizungushia uchungu na mateso. Amenikalisha gizani kama watu waliokufa zamani. Amenizungushia ukuta nisitoroke, amenifunga kwa minyororo mizito. Ingawa naita na kulilia msaada anaizuia sala yangu isimfikie. Njia zangu ameziziba kwa mawe makubwa amevipotosha vichochoro vyangu. Yeye ni kama dubu anayenivizia; ni kama simba aliyejificha. Alinifukuza njiani mwangu, akanilemaza na kuniacha mkiwa. Aliuvuta upinde wake, akanilenga mshale wake. Alinichoma moyoni kwa mishale, kutoka katika podo lake. Nimekuwa kitu cha dhihaka kwa watu wote, mchana kutwa nimekuwa mtu wa kuzomewa. Amenijaza taabu, akanishibisha uchungu. Amenisagisha meno katika mawe, akanifanya nigaegae majivuni. Moyo wangu haujui tena amani, kwangu furaha ni kitu kigeni. Nimewaza “Nimekata tamaa kabisa, tumaini langu kwa Mwenyezi-Mungu limetoweka.” Kukumbuka taabu na kutangatanga kwangu kwanipa uchungu kama wa nyongo. Nayafikiria hayo daima, nayo roho yangu imejaa majonzi. Lakini nakumbuka jambo hili moja, nami ninalo tumaini: Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno. Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu hivyo nitamwekea tumaini langu. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea, ni mwema kwa wote wanaomtafuta. Ni vema mtu kungojea kwa saburi ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu. Ni vema mtu kujifunza uvumilivu tangu wakati wa ujana wake. Heri kukaa peke na kimya, mazito yanapompata kutoka kwa Mungu. Yampasa kuinama na kujinyenyekesha, huenda ikawa tumaini bado lipo. Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga, na kuwa tayari kupokea matusi yake. Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu. Wafungwa wote nchini wanapodhulumiwa na kupondwa; haki za binadamu zinapopotoshwa mbele yake Mungu Mkuu, kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani, je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo? Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo? Maafa na mema hutokea tu kwa amri yake Mungu Mkuu. Kwa nini mtu anung'unike, ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake?