Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 32:17-35

Yeremia 32:17-35 BHN

Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako. Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako. Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake. Katika nchi ya Misri ulifanya maajabu, ukatenda miujiza, na unaendelea kufanya hivyo mpaka leo miongoni mwa Waisraeli na katika mataifa mengine pia, jambo ambalo limekufanya ujulikane kila mahali. Kwa maajabu na miujiza uliyowatisha nayo Wamisri, uliwatoa watu wako Misri kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Tazama, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa watu wote. Hakuna lolote linaloweza kunishinda. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninautoa mji huu kwa Wakaldayo na kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Wakaldayo wanaoushambulia mji huu wataingia na kuuchoma moto; watauteketeza pamoja na nyumba ambazo juu ya paa zake ubani ulifukiziwa mungu Baali na tambiko za divai zilimiminiwa miungu mingine, ili kunichokoza. Maana Waisraeli na watu wa Yuda hawakufanya chochote mbele yangu isipokuwa uovu tangu ujana wao; watu wa Israeli hawakufanya chochote isipokuwa kunikasirisha kwa matendo yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mji huu umechochea hasira yangu na kuniudhi tangu siku ulipojengwa mpaka leo hii. Kwa hiyo, nitautoa kabisa mbele yangu, kwa sababu ya uovu wote waliotenda watu wa Israeli na watu wa Yuda, pamoja na wafalme na viongozi wao, makuhani na manabii wao, na wakazi wa Yerusalemu. Wao walinipa kisogo badala ya kunigeuzia nyuso zao; ingawa nimewafundisha tena na tena, wao hawakusikiliza na kuyapokea mafundisho yangu. Waliweka sanamu za miungu yao ya kuchukiza katika nyumba hii inayojulikana kwa jina langu, wakaitia unajisi. Walimjengea mungu Baali madhabahu katika bonde la Mwana wa Hinomu, ili wamtolee mungu Moleki wavulana wao na binti zao, ingawa sikuwaamuru wala sikufikiria kwamba wangefanya hivyo, wakawafanya watu wa Yuda watende dhambi.”

Soma Yeremia 32

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha