Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9:1-19

Danieli 9:1-19 BHN

“Katika mwaka Dario mwana wa Ahasuero, Mmedi, alipoanza kutawala juu ya milki ya Wakaldayo, mimi Danieli nilikuwa nikivisoma kwa makini vitabu vitakatifu, na humo nikaelewa maana ya jambo lile Mwenyezi-Mungu alilomfahamisha nabii Yeremia kuhusu ile miaka sabini, muda ambao utahusika na kuharibiwa kwa Yerusalemu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema: “Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako. Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako. Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako waliongea na wafalme wetu, wakuu wetu, wazee wetu na taifa letu lote. Kwako, ee Bwana, kuna uadilifu, lakini sisi daima tumejaa aibu. Jambo hili ni kweli kwetu sote tuishio Yudea, wakazi wa mji wa Yerusalemu na Waisraeli wote ambao umewatawanya katika nchi za mbali na za karibu kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako. Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea. Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi. Tulikataa kukusikiliza, ee Bwana, Mungu wetu; hatukuishi kulingana na sheria zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii. Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako. Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani. Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako. Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza. “Na sasa ee Bwana, Mungu wetu, uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa nguvu yako kuu na kulifanya jina lako litukuke mpaka sasa, tunasema kwamba tumetenda dhambi; tumefanya maovu. Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki usiukasirikie wala kuughadhibikia mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Watu wote wa nchi za jirani wanaudharau mji wa Yerusalemu na watu wako, kwa sababu ya dhambi zetu na maovu waliyotenda wazee wetu. Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa. Tega sikio, ee Mungu wangu; angalia uone taabu tulizo nazo na jinsi unavyotaabika huo mji uitwao kwa jina lako. Tunakutolea maombi yetu si kwa sababu tumetenda haki, bali kwa sababu wewe una huruma nyingi. Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako!

Soma Danieli 9

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Danieli 9:1-19

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha