Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 17:12-40

1 Samueli 17:12-40 BHN

Daudi alikuwa mtoto wa Yese, Mwefrathi kutoka Bethlehemu katika Yuda. Yese alikuwa na watoto wanane wa kiume. Wakati Shauli alipokuwa mfalme, yeye alikuwa tayari mzee, mtu mwenye umri mkubwa. Wana wakubwa watatu wa Yese, Eliabu mzaliwa wa kwanza, Abinadabu aliyefuata na Shama wa tatu, walikuwa wamekwenda pamoja na Shauli vitani. Daudi alikuwa ndiye mdogo wa wote. Wale watoto watatu wakubwa walikuwa wamekwenda na Shauli. Ingawa Daudi mara kwa mara alikwenda kwa Shauli, alirudi nyumbani Bethlehemu kuchunga kondoo wa baba yake. Kwa muda wa siku arubaini, asubuhi na jioni, yule Mfilisti Goliathi alijitokeza hadharani, akasimama na kuwakejeli wanajeshi wa Israeli. Siku moja, Yese alimwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako bisi kilo kumi na mikate kumi. Wapelekee haraka huko kambini. Na yule kamanda wao wa kikosi cha wanajeshi elfu mpelekee jibini hizi kumi. Kawaangalie kaka zako kama wanaendelea vizuri na kisha uniletee habari zao.” Wakati huo mfalme Shauli, kaka zake Daudi na wanajeshi wote wa Israeli walikuwa kwenye bonde la Ela, wanapigana na Wafilisti. Kesho yake, Daudi aliamka asubuhi na mapema, na kondoo akamwachia mchungaji. Alichukua chakula na kwenda kama alivyoagizwa na baba yake Yese. Alipofika kwenye kambi ya Waisraeli, aliwakuta wanajipanga kwenye sehemu yao ya vita na wanapiga kelele za vita. Majeshi ya Waisraeli na ya Wafilisti walijipanga tayari kupigana vita, majeshi yakiwa yanakabiliana ana kwa ana. Daudi alimkabidhi chakula mtu aliyetunza mizigo, akawakimbilia wanajeshi, akaenda kwa kaka zake na kuwasalimia. Alipokuwa anaongea nao, Goliathi yule shujaa wa Wafilisti kutoka Gathi alijitokeza mbele ya wanajeshi wa Israeli kama alivyozoea. Naye Daudi alimsikiliza vizuri sana. Waisraeli walipomwona Goliathi, walimkimbia, na kumwogopa sana. Waliambiana, “Je, mmemwona yule mtu aliyejitokeza? Ama kweli, amejitokeza kuwakejeli Waisraeli. Mfalme Shauli atampa mtu yeyote atakayemuua mtu huyo utajiri mwingi. Zaidi ya yote, atamwoza binti yake. Tena, watu wa jamaa ya baba yake watakuwa huru, hawatalipa kodi.” Daudi akawauliza wale waliokuwa karibu naye, “Je, mtu atakayemuua Mfilisti huyu na kuikomboa Israeli kutokana na aibu hii atafanyiwa nini? Ni nani huyu Mfilisti, mtu asiyetahiriwa, anayethubutu kuyatukana majeshi ya Mungu aliye hai?” Watu wakamwambia kama walivyokuwa wamesema hapo awali juu ya mtu atakayemuua Goliathi. Lakini Eliabu, kaka mkubwa wa Daudi alipomsikia Daudi akiongea na watu, alimkasirikia Daudi, akasema, “Kwa nini umekuja? Je, wale kondoo wachache umemwachia nani kule nyikani? Najua ujeuri wako na uovu wako. Umekuja tu kutazama vita.” Daudi akamjibu, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi kuuliza swali tu?” Daudi akamgeukia mtu mwingine akamwuliza swali hilohilo; na kila alipouliza, alipata jibu lilelile. Watu fulani ambao walimsikia Daudi alivyosema, walikwenda kumwambia Shauli. Naye Shauli akaagiza aitwe. Daudi akamwambia Shauli, “Mtu yeyote asitishike moyoni mwake kutokana na Mfilisti huyu. Mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana naye.” Shauli akamwambia Daudi, “Wewe huwezi kwenda kupigana na Mfilisti yule. Wewe ni kijana tu, lakini mtu huyo amekuwa vitani tangu ujana wake.” Daudi akasema, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu.” Shauli akamwambia, “Nenda; naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nawe.” Shauli akamvisha Daudi mavazi yake ya kivita, akamvika kofia yake ya shaba kichwani na koti lake la kujikinga kifua. Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua. Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Samueli 17:12-40

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha