Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 15:14-28

1 Samueli 15:14-28 BHN

Samueli akamwambia, “Mbona nasikia mlio wa kondoo na ng'ombe?” Shauli akajibu, “Watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe bora kabisa ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, lakini wengine wote tumewaangamiza.” Samueli akamkatiza Shauli, “Nyamaza! Nitakuambia jambo aliloniambia Mwenyezi-Mungu leo usiku.” Shauli akasema, “Niambie.” Samueli akamwambia, “Ingawa unajiona kuwa wewe si maarufu, je, wewe si kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi-Mungu alikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Mwenyezi-Mungu alipokutuma alikuambia, ‘Nenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hadi umewaua wote!’ Kwa nini basi, hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini mkakimbilia nyara na hivyo kutenda jambo ovu mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Shauli akajibu, “Nimetii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Nilikwenda kule alikonituma Mwenyezi-Mungu; nimemleta Agagi mfalme wa Waamaleki, na nimewaangamiza kabisa Waamaleki. Lakini watu walichukua nyara: Kondoo, ng'ombe na vitu vyote bora vilivyotolewa viangamizwe ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.” Ndipo Samueli akamwambia, “Je, Mwenyezi-Mungu anapendelea zaidi dhabihu za kuteketezwa na matambiko, kuliko kuitii sauti yake? Tazama, kumtii yeye ni bora kuliko matambiko na kumsikiliza kuliko kumtambikia mafuta ya beberu. Uasi ni sawa na dhambi ya kupiga ramli, na kiburi ni sawa na uovu na kuabudu vinyago. Kwa sababu umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme.” Shauli akamwambia Samueli, “Nimetenda dhambi. Nimeasi amri ya Mwenyezi-Mungu na amri yako, kwa sababu niliwaogopa watu, nikawatii wao. Lakini sasa nakuomba, unisamehe dhambi yangu. Niruhusu nirudi pamoja nawe ili niweze kumwabudu Mwenyezi-Mungu.” Samueli akamjibu: “Kamwe, siwezi kurudi pamoja nawe. Wewe umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme juu ya Israeli.” Samueli alipogeuka ili aende zake, Shauli akashika pindo la vazi lake, nalo likapasuka. Ndipo Samueli alipomwambia Shauli, “Tangu leo Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako na atampa mtu mwingine miongoni mwa jirani zako aliye bora kuliko wewe.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha