Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 15:1-13

1 Samueli 15:1-13 BHN

Samueli alimwambia Shauli, “Mwenyezi-Mungu alinituma kukupaka mafuta uwe mfalme wa watu wake wa Israeli. Sasa sikiliza maneno ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa sababu waliwapiga Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri. Sasa, nenda ukawashambulie na kuangamiza vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache hai, ila uwaue wote: Wanaume kwa wanawake, watoto wachanga na wanyonyao, ng'ombe, kondoo, ngamia na punda.’” Shauli akaliita jeshi lake, akalikagua huko Telaimu. Kulikuwa na askari wa miguu 200,000 kutoka Israeli na 10,000 kutoka Yuda. Halafu yeye na watu wake wakaenda kwenye mji wa Amaleki, wakawa wakivizia kwenye bonde. Shauli akawaambia Wakeni, “Nendeni! Ondokeni! Tokeni miongoni mwa Waamaleki, la sivyo, nitawaangamiza pamoja nao. Ondokeni kwa sababu nyinyi mliwatendea wema Waisraeli walipotoka Misri.” Basi, Wakeni wakaondoka miongoni mwa Waamaleki. Shauli aliwashinda Waamaleki kuanzia Havila hadi Shuri, mashariki ya Misri. Alimteka mfalme Agagi wa Waamaleki akiwa hai. Akawaua watu kwa makali ya upanga. Lakini Shauli na watu wake hawakumuua Agagi, wala kondoo bora kabisa, ng'ombe wazuri, ndama, wanakondoo na chochote kile kilichokuwa kizuri hawakukiangamiza. Lakini vitu vyote vibaya na visivyo na thamani waliviangamiza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Ninajuta kwamba nimemfanya Shauli kuwa mfalme. Yeye ameacha kunifuata mimi na hajatimiza amri zangu.” Samueli alikasirika, akamlilia Mwenyezi-Mungu usiku kucha. Samueli alisikia kuwa Shauli alikuwa amekuja huko Karmeli na amesimamisha mnara wa ukumbusho wake, na kwamba amekwenda Gilgali. Hivyo, kesho yake, Samueli aliamka asubuhi na mapema akaenda kukutana na Shauli. Samueli alipomfikia Shauli, Shauli akamwambia Samueli, “Mwenyezi-Mungu na akubariki! Nimetekeleza amri ya Mwenyezi-Mungu.”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha