Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wakolosai 1

1
1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo,#1:1 Timotheo: Taz 2Kor 1:1 maelezo. 2tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu#1:2 Watu wa Mungu: Taz Rom 1:7; rejea Efe 1:1; Fil 1:1. Tafsiri nyingine “watakatifu”. huko Kolosai,#1:2 Kolosai: Mji katika mkoa wa Kiroma wa Asia, katika eneo la Frugia; hivi sasa ni sehemu ya nchi ya Uturuki. Kolosai ulikuwa yapata kilomita 175 magharibi mwa mji wa Efeso. Paulo akiwa kule Efeso, wakati wa safari yake ya tatu ya kuhubiri Injili, alimtuma Epafra huko Kolosai; taz Kol 1:7. Rejea pia Mate 19:10 maelezo, na Kol 4:12. ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.#1:1-2 Kuhusu namna ya kuanza kuandika barua nyakati hizo, taz Rom 1:1-7, maelezo na Utangulizi kwa Barua za A.J.
Sala ya shukrani
3Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. 4Maana tumesikia juu ya imani yenu kwa Kristo Yesu na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. 5Imani yenu na mapendo yenu vina msingi katika tumaini mlilowekewa mbinguni.#1:5 Tumaini mlilowekewa mbinguni: 1Pet 1:4. Mlipata kusikia juu ya hilo tumaini mara ya kwanza wakati mlipohubiriwa ule ujumbe wa ukweli wa Habari Njema. 6Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote#1:6 Ulimwenguni kote: Yaani walau kama ulivyojulikana wakati huo. kama vile ilivyofanya kwenu nyinyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. 7Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra,#1:7 Epafra: Mkazi wa Kolosai ambaye alikuwa pamoja na Paulo wakati huo (Kol 4:12; File 23); taz Kol 1:2, maelezo; na utangulizi kwa barua hii. mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. 8Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. 9Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu wakati tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa matakwa yake, pamoja na hekima yote na ujuzi wa kiroho. 10Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. 11Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. 12Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga.#1:12-14 Rejea Mate 26:18. 13Yeye alituokoa katika nguvu ya giza,#1:13 Nguvu ya giza: Au, nguvu za uovu. Yaani, utawala wa Shetani; rejea Efe 6:12 na taz Luka 22:53, maelezo. akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi.#1:13 Mwanae mpenzi: Taz Efe 1:6 maelezo. 14Kwake yeye tunakombolewa,#1:14 Tunakombolewa: Taz Rom 3:24, maelezo. yaani dhambi zetu zinaondolewa.#1:14 Dhambi zetu zinaondolewa: Efe 1:7.
Kristo na kazi yake
15Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana;
ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.#1:15 Mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote: Yaani yeye alitangulia kuweko kwa viumbe. Jina “Mzaliwa wa kwanza” (taz Luka 2:7, maelezo) linatumika kutilia mkazo pia juu ya jambo la Yesu Kristo kuchukua nafasi ya kwanza kabisa. Kwa kusema hivyo mwandishi anazikabili pia fikra za wale waliofundisha huko Kolosai kwamba kuna roho nyingine au nguvu zilizo kati ya Mungu na binadamu, ambazo ni lazima ziabudiwe (taz Utangulizi). Rejea Yoh 1:1-2; 2Kor 4:4; Ebr 1:2-4.
16Maana kwake vitu vyote viliumbwa
kila kitu duniani na mbinguni,
vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:
wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu.#1:16 Wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu: Rejea Efe 1:21; 6:12. Wakati huo, bila Habari Njema ya Yesu, ilifikiriwa kwamba hao wanaotajwa hapa walikuwa wajumbe kati ya Mungu na ulimwengu. Paulo anasema sivyo ila Yesu Kristo ndiye aliye juu ya yote.
Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake.#1:16 Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake: Rejea Yoh 1:3; 1Kor 8:6. Yale yanayosemwa katika Meth 8:22-33 juu ya hekima kwamba ilikuwako kabla ya vitu vyote na kushiriki kwake katika kuumba ulimwengu, sasa yanasemwa kuhusu Yesu Kristo.
17Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote;
vyote huendelea kuwako kwa uwezo wake.#1:17 Yoh 1:1-3; 8:58; Ebr 1:2-3. mstari wa pili wa aya hii unasisitiza kwamba Mungu huendelea kuvitegemeza vitu kwa njia Kristo.
18Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa;#1:18 Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa: Efe 1:22-23; 5:23.
yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili.
Yeye ndiye mwanzo,
mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka kwa wafu,
ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.
19Maana Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake.#1:19 Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake: Utimilifu wake Mungu ni uwezo na nguvu zake katika kuumba na kutegemeza viumbe vyake. Neno hili “utimilifu” linatumika pia katika Efe 1:23; 3:19; 4:13 na Kol 2:9, lakini mazingira ya maandishi ambamo linatumika yanaweza kulipa maana yake tofauti.
20Kwake vitu vyote vilipatanishwa na Mungu:
na kwa damu yake#1:20 Kwa damu yake: Efe 2:16; taz Efe 1:7, maelezo. msalabani#1:20 Msalabani: Efe 1:10; rejea 2Kor 5:18-19; rejea pia Rom 8:19-23. akafanya amani
na vitu vyote duniani na mbinguni.#1:15-20 Sehemu hii ya 1:15-20 ni utenzi au wimbo ambao unatangaza ukuu wake Kristo katika uhusiano wake na Mungu, uhusiano wake na viumbe vyote, lakini hasa na kanisa ambalo ni mwili wake. Katika utenzi huu kazi yake ya ukombozi pia inatiliwa mkazo. Yamkini utenzi huu msingi wake ni wimbo fulani uliotumika wakati fulani katika ibada ya kanisa (rejea pia Yoh 1:1-18; Fil 2:6-11; 1Tim 3:16; Ebr 1:1-4).
21Hapo kwanza nyinyi#1:21 Nyinyi: Yaani, waumini ambao si Wayahudi. Kwamba “walikuwa mbali na watu wa Mungu”, taz Efe 2:12-13, na kwamba “walikuwa adui wa Mungu”, taz Rom 5:10. pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. 22Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha#1:22 Amewapatanisha: Taz 2Kor 5:18-20 maelezo; rejea Efe 2:13-16. naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama.#1:22 Watakatifu, safi na bila lawama: Taz Efe 1:4 maelezo; rejea Efe 5:27. 23Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani.#1:23 Injili …imekwisha hubiriwa kila mtu duniani: Taz maelezo ya aya ya 6, na rejea pia Marko 16:15.
Huduma ya Paulo katika makanisa
24Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo#1:24 Kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo: Ili isieleweke kana kwamba mateso ya Kristo hayakutosha kwa wokovu, inafaa kusema kwamba katika kuitwa kumtumikia Kristo watumishi wake ni lazima wateseke kama yeye; mateso ni jambo muhimu katika kumtumikia Kristo. kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa. 25Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake, 26ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake.#1:26-27 Rom 8:10; Efe 3:17; Kol 2:2; 4:3. Kuhusu “siri”, taz Efe 1:9. 27Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu,#1:27 Kristo yuko ndani yenu: Rom 8:10; Efe 3:17. na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu. 28Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo. 29Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.

Iliyochaguliwa sasa

Wakolosai 1: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia