Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 7:1-9

Waamuzi 7:1-9 SRUV

Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka asubuhi na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno kwangu kuwatia Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu yeyote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu elfu ishirini na mbili wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; walete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. Basi Gideoni akachukua vyakula vyao na tarumbeta zao, kisha akawaaga watu wote wa Israeli, kila mtu hemani mwake; akabaki na watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako.

Soma Waamuzi 7