Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 11:16-33

2 Wakorintho 11:16-33 SRUV

Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu angaa kidogo. Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu. Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu. Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha. Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni. Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Lakini, ikiwa mtu anao ujasiri kwa lolote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Abrahamu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nilipata mapigo arubaini kasoro moja. Mara tatu nilipigwa kwa bakora; mara moja nilipigwa kwa mawe; mara tatu nilivunjikiwa jahazi; kutwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Mbali na mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski mtawala wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikateremshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wakorintho 11:16-33

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha