Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 37

37
Hezekia Aomba Ushauri kwa Isaya
1 # 2 Fal 19:1; 2 Nya 6:24; Zab 50:15; Zek 13:9; Lk 18:1; Rum 12:12; 1 The 5:17 Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA. 2#2 Fal 22:14Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. 3#2 Fal 19:3; Hos 5:9; Zab 39:11; 50:15Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa. 4#1 Sam 7:8; 2 Fal 19:4; Yak 5:14,18Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia. 5Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya. 6Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. 7Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8 # Yos 15:39,42; 2 Nya 11:9; Neh 11:30; Yer 34:7 Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi. 9Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema, 10Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. 11Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe? 12#Mwa 11:31Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? 13#Yer 49:23Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva?
Ombi la Hezekia
14Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. 15Hezekia akamwomba BWANA, akisema, 16#Kut 25:22Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. 17#Dan 9:18Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. 18Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, 19na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. 20Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.
21Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, 22tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili; Bikira, binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake juu yako. 23Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli. 24Umemshutumu Bwana kwa watumishi wako, kwa kuwa umesema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani ya Lebanoni; nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri, nami nitaingia ndani ya mahali pake palipoinuka, palipo mbali sana, msitu wa shamba lake lizaalo sana. 25Nimechimba na kunywa maji, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri. 26Je! Hukusikia? Ni mimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale; nikayatimiza sasa, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, ikawe chungu na magofu. 27Ndiyo sababu wenyeji wao wakawa hawana nguvu, na kufadhaika, na kuhangaika, wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, kama shamba la ngano kabla haijaiva. 28Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako uliyonighadhibikia. 29#Ayu 41:2; Zab 32:9; Isa 30:28; Eze 29:4; Amo 4:2; Yak 3:3Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu, nitatia kulabu yangu katika pua yako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha kwa njia ile ile uliyoijia. 30Na kwako wewe dalili ndiyo hii; mwaka huu mtakula vitu vimeavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya mbegu za vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mizabibu katika mashamba, mkale matunda yake. 31Na mabaki yaliyookoka, yaliyobakia ya nyumba ya Yuda, yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. 32#2 Fal 19:31Maana katika Yerusalemu yatatoka mabaki, nao watakaookoka katika mlima Sayuni; wivu wa BWANA wa majeshi utatimiza mambo hayo. 33Basi, BWANA asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hataingia ndani ya mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. 34Njia ile ile aliyoijia, kwa njia hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu; asema BWANA. 35#2 Fal 20:6; Isa 27:3Nami nitaulinda mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.
Kushindwa na Kuuawa kwa Senakeribu
36 # 2 Fal 19:35 Basi malaika wa BWANA alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia. 37Basi Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaenda zake, akarudi Ninawi, akakaa huko. 38Ikawa alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza, wanawe, wakampiga kwa upanga; wakakimbilia nchi ya Ararati; naye Esar-hadoni, mwanawe, akamiliki badala yake.

Iliyochaguliwa sasa

Isa 37: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha