Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kut 32:1-20

Kut 32:1-20 SUV

Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee. Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa BWANA. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze. BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake. Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi. Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli.

Soma Kut 32

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kut 32:1-20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha