Wafilipi 2:17-23
Wafilipi 2:17-23 NENO
Lakini hata nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma inayotoka katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami. Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi. Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo. Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake. Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa.