Wafilipi 1:1-26
Wafilipi 1:1-26 NENO
Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu. Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu walio Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu. Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami. Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu. Haya ndio maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kupitia kwa Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu. Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo. Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga. Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema. Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili. Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu. Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi. Naam, nami nitaendelea kufurahi, kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini nichague lipi? Mimi sijui! Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi. Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili. Nikiwa na hakika ya jambo hili, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani, ili kwa kuja kwangu kwenu tena, furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu.