Hesabu 27:1-11
Hesabu 27:1-11 NENO
Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yusufu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Musa, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema, “Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya BWANA, lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana. Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.” Kwa hiyo Musa akaleta shauri lao mbele za BWANA, naye BWANA akamwambia Musa, “Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa. Ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao. “Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama BWANA alivyomwamuru Musa.’ ”