Mathayo 27:46-54
Mathayo 27:46-54 NEN
Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.” Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake. Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi. Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”





