Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 26:1-25

Mathayo 26:1-25 NENO

Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.” Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. Wakapanga kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.” Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula. Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.” Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.” Kisha mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alienda kwa viongozi wa makuhani na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu. Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” Hivyo wanafunzi wakafanya vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!” Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?” Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”