Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 22:15-33

Mathayo 22:15-33 NENO

Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. Wakatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode kwake. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonesha upendeleo. Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Yesu alifahamu kusudi lao mbaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? Nionesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao. Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema, “Mwalimu, Musa alisema, ‘Mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?” Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Wale umati wa watu waliposikia hayo, walishangaa sana kwa mafundisho yake.