Luka 4:38-43
Luka 4:38-43 NENO
Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani mwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie. Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka mara moja, naye akaanza kuwahudumia. Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Yesu watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya. Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Kristo. Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alienda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke. Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”