Luka 12:49-59
Luka 12:49-59 NENO
“Nimekuja kuleta moto duniani; laiti kama ungekuwa tayari umewashwa! Lakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu hadi ubatizo huo ukamilike! Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano. Kuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, naye mama mkwe dhidi ya mkwewe na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.” Pia Yesu akaambia umati ule wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha. Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo. Enyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa? “Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki? Ukiwa njiani na mshtaki wako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani. Nakuambia, hutatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.”