Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 3:1-39

Maombolezo 3:1-39 NENO

Mimi ndiye mtu aliyeona mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake. Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee gizani wala si katika nuru; hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu tena na tena, mchana kutwa. Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa na ameivunja mifupa yangu. Amenizingira na kunizunguka kwa uchungu na taabu. Amenifanya niishi gizani kama wale waliokufa. Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito. Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu. Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu. Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni, ameniburuta kutoka njiani, akanirarua na kuniacha bila msaada. Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake. Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake. Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa. Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo. Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini. Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini. Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa BWANA.” Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo. Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu. Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini. Kwa sababu ya upendo mkuu wa BWANA, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe. Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu. Nimeiambia nafsi yangu, “BWANA ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.” BWANA ni mwema kwa wale wanaomtumaini, na kwa yule anayemtafuta; ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa BWANA. Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana. Na akae peke yake awe kimya, kwa maana BWANA ameiweka juu yake. Hata azike uso wake mavumbini bado tumaini litakuwepo. Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu. Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele. Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu. Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu. Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi, Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana, kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya? Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru? Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema? Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?