Isaya 6:1-6
Isaya 6:1-6 NENO
Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi kwenye kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. Juu yake walikuwa maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi. Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi kati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.” Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.