Isaya 5:8-30
Isaya 5:8-30 NENO
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi. BWANA wa majeshi amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa. Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja ya divai, na homeri moja ya mbegu zilizopandwa itatoa efa moja tu ya nafaka.” Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana hadi usiku, hata wamewaka kwa mvinyo. Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya BWANA, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake. Kwa hiyo watu wangu wataenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa maarifa; watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa, nao watu wengi watakauka kwa kiu. Kwa hiyo Kaburi limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani yake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote. Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa. Lakini BWANA wa majeshi atatukuzwa kwa ajili ya haki yake, naye Mungu Mtakatifu atajionesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa haki yake. Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe, wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri. Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu na uovu kama kwa kamba za mkokoteni, kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka, aharakishe kazi yake ili tupate kuiona. Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike, tena udhihirike ili tupate kuujua.” Ole wao wanaoita ubaya ni wema, na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu. Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe, na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe. Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo, nao walio hodari katika kuchanganya vileo, wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia. Kwa hiyo, kama ndimi za moto zinavyoteketeza nyasi, na kama vile majani makavu yanavyozama katika miali ya moto, ndivyo mizizi yao itakavyooza, na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi; kwa kuwa wameikataa sheria ya BWANA wa majeshi na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli. Kwa hiyo hasira ya BWANA inawaka dhidi ya watu wake, mkono wake umeinuliwa na anawapiga. Milima inatetemeka, maiti ni kama takataka kwenye barabara. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali, anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia. Tazama wamekuja, kwa kasi na kwa haraka! Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa, hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala, hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni, hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika. Mishale yao ni mikali, pinde zao zote zimevutwa, kwato za farasi wao ziko kama gumegume, magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli. Ngurumo yao ni kama ile ya simba, wananguruma kama wana simba, wanakoroma wanapokamata mawindo yao, na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa. Katika siku ile watanguruma juu yake kama ngurumo za bahari. Kama mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki; hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.