Isaya 45:9-25
Isaya 45:9-25 NENO
“Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake, yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi. Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi, ‘Unatengeneza nini wewe?’ Je, kazi yako husema, ‘Hana mikono’? Ole wake amwambiaye baba yake, ‘Umezaa nini?’ Au kumwambia mama yake, ‘Umezaa kitu gani?’ “Hili ndilo asemalo BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu? Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani. Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu: nitazinyoosha njia zake zote. Yeye atajenga mji wangu upya, na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni, lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi, nao wale Waseba warefu, watakujia na kuwa wako, watakujia wakijikokota nyuma yako, watakujia wamefungwa minyororo. Watasujudu mbele yako, wakikusihi na kusema, ‘Hakika Mungu yu pamoja nawe, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine.’ ” Hakika wewe u Mungu unayejificha, Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli. Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika; wataenda kutahayarika pamoja. Lakini Israeli ataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; kamwe hutaaibika wala kutatahayarika, milele yote. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Anasema: “Mimi ndimi BWANA, wala hakuna mwingine. Sijasema sirini, kutoka mahali fulani katika nchi ya giza; sijawaambia wazao wa Yakobo, ‘Nitafuteni bure.’ Mimi, BWANA, nasema kweli; ninatangaza lililo sahihi. “Kusanyikeni pamoja mje, enyi wakimbizi kutoka mataifa. Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili, wale waombao miungu isiyoweza kuokoa. Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo; wao na wafanye shauri pamoja. Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani, aliyelitangaza tangu zamani za kale? Je, haikuwa Mimi, BWANA? Wala hapana Mungu mwingine zaidi yangu mimi, Mungu mwenye haki na Mwokozi; hapana mwingine ila mimi. “Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe, enyi miisho yote ya dunia; kwa maana mimi ndimi Mungu, wala hapana mwingine. Nimeapa kwa nafsi yangu, kinywa changu kimenena katika uadilifu wote neno ambalo halitatanguka: Kila goti litapigwa mbele zangu, kwangu mimi kila ulimi utaapa. Watasema kunihusu, ‘Katika BWANA peke yake ndiko kuna haki na nguvu.’ ” Wote ambao wamemkasirikia Mungu watamjia yeye, nao watatahayarika. Lakini katika BWANA wazao wote wa Israeli wataonekana wenye haki na watashangilia.