Isaya 33:1-12
Isaya 33:1-12 NENO
Ole wako wewe, ee mharibu, wewe ambaye hukuharibiwa! Ole wako, ee msaliti, wewe ambaye hukusalitiwa! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa; utakapokwisha kusaliti, utasalitiwa. Ee BWANA, uturehemu, tunakutamani. Uwe nguvu yetu kila asubuhi na wokovu wetu wakati wa taabu. Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia; unapoinuka, mataifa hutawanyika. Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama wafanyavyo madumadu, watu huvamia juu yake kama kundi la nzige. BWANA ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka, ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu. Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu, hazina ya wokovu tele, hekima na maarifa; kumcha BWANA ni ufunguo wa hazina hii. Angalia, mashujaa wake wanapiga kelele barabarani, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. Njia kuu zimeachwa, hakuna wasafiri barabarani. Mkataba umevunjika, mashahidi wake wamedharauliwa, hakuna anayeheshimiwa. Ardhi inaomboleza na kuchakaa, Lebanoni imeaibika na kunyauka; Sharoni ni kama Araba, nayo Bashani na Karmeli wanapukutisha majani yao. “Sasa nitainuka,” asema BWANA. “Sasa nitatukuzwa; sasa nitainuliwa juu. Mlichukua mimba ya makapi, mkazaa mabua; pumzi yenu ni moto unaowateketeza. Mataifa watachomwa wawe majivu; kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”


