Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 12:12-29

Waebrania 12:12-29 NEN

Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea. Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe. Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana. Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi. Hamjaufikia mlima ule uwezao kuguswa na ambao unawaka moto; wala kwenye giza, utusitusi na dhoruba; kwenye mlio wa tarumbeta, au kwenye sauti isemayo maneno ya kutisha kiasi ambacho wale walioisikia waliomba wasiambiwe neno jingine zaidi, kwa sababu hawangeweza kustahimili neno lile lililoamriwa: “Hata kama mnyama atagusa mlima huu, atapigwa mawe.” Waliyoyaona yalikuwa ya kutisha kiasi kwamba Mose alisema, “Ninatetemeka kwa hofu.” Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa, kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli. Angalieni, msije mkamkataa yeye anenaye. Ikiwa wao hawakuepuka adhabu walipomkataa yeye aliyewaonya hapa duniani, sisi je, tutaokokaje tusipomsikiliza yeye anayetuonya kutoka mbinguni? Wakati ule sauti yake ilitetemesha dunia, lakini sasa ameahidi, “Kwa mara moja tena nitatetemesha si nchi tu bali na mbingu pia.” Maneno haya “kwa mara moja tena” yanaonyesha kuondoshwa kwa vile vitu vinavyoweza kutetemeshwa, yaani vile vitu vilivyoumbwa, kwa kusudi vile tu visivyoweza kutetemeshwa vibaki. Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji, kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha