Hagai 2:10-19
Hagai 2:10-19 NENO
Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa nabii Hagai: “Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema: Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ” Makuhani wakajibu, “La.” Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?” Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.” Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema BWANA. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi. “ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la BWANA. Mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu. Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema BWANA. ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la BWANA uliwekwa. Tafakarini: Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Hadi sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda. “ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”