Mwanzo 35:16-29
Mwanzo 35:16-29 NENO
Kisha wakaondoka Betheli. Kabla hawajafika Efrata, Raheli akaanza kujifungua na akapata shida kuu. Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.” Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe jina Benoni. Lakini babaye akamwita jina Benyamini. Kwa hiyo Raheli akafa, na akazikwa kando ya njia iendayo Efrata (ndio Bethlehemu). Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ambayo hadi leo inatambulisha kaburi la Raheli. Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema baada ya kupita Mnara wa Ederi. Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aliyeitwa Bilha, naye Israeli akasikia jambo hilo. Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili: Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni. Wana wa Raheli walikuwa: Yusufu na Benyamini. Wana waliozaliwa na Bilha mjakazi wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali. Wana waliozaliwa na Zilpa mjakazi wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri. Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu. Yakobo akarudi nyumbani mwa baba yake Isaka huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaka. Isaka aliishi miaka mia moja na themanini. Kisha Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho, akafa; akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee aliyeshiba siku. Nao Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.