Mwanzo 21:1-13
Mwanzo 21:1-13 NENO
Wakati huu BWANA akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na BWANA akamtendea Sara kama alivyoahidi. Sara akapata mimba, na akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi. Abrahamu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka. Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa. Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.” Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa. Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki. Hivyo Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.” Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe. Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”