Mwanzo 19:12-29
Mwanzo 19:12-29 NENO
Wale wanaume wawili wakamwambia Lutu, “Una mtu mwingine yeyote hapa: wakwe, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa BWANA dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.” Kwa hiyo Lutu alitoka ili kuzungumza na wakwe wake waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa BWANA yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe wake walifikiri kwamba alikuwa akitania. Kulipopambazuka, malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walio huku, la sivyo utaangamizwa mji huu utakapoadhibiwa.” Alipositasita, wale wanaume wakamshika mkono wake, na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa BWANA aliwahurumia. Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!” Lakini Lutu akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani; janga hili litanikumba, nami nitakufa. Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo: Ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.” Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote hadi ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.) Lutu alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. Ndipo BWANA akanyesha moto wa kiberiti juu ya Sodoma na Gomora kutoka kwake BWANA mbinguni. Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote walioishi katika miji hiyo, hata pia mimea yote katika nchi. Lakini mke wa Lutu akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi. Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Abrahamu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za BWANA. Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka nchi, kama moshi unaotoka katika tanuru. Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare, alimkumbuka Abrahamu, akamtoa Lutu kutoka lile janga lililoharibu miji ile ambamo Lutu alikuwa ameishi.