Kutoka 3:1-9
Kutoka 3:1-9 NENO
Basi Musa alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Musa akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu. Huko malaika wa BWANA akamtokea Musa katika mwali wa moto kutoka kichakani. Musa akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. Ndipo Musa akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.” BWANA alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Musa! Musa!” Naye Musa akajibu, “Mimi hapa.” Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Kisha akamwambia, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Musa aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu. BWANA akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami nimeguswa na mateso yao. Basi nimeshuka niwaokoe kutoka mkono wa Wamisri, niwatoe na kuwapandisha kutoka nchi hiyo, niwapeleke katika nchi nzuri na kubwa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Sasa kilio cha Waisraeli kimenifikia, nami nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa.