Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 29:10-28

Kutoka 29:10-28 NENO

“Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje huyo fahali mbele za BWANA kwenye mlango wa Hema la Kukutania. Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu. Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, na kipande kirefu cha ini, na figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu. Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi. “Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu. Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine. Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Haruni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Haruni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu. Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Haruni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Haruni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu. “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani, kipande kirefu cha ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.) Kutoka kwa kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za BWANA, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta, na mkate mwembamba. Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe na uviinue mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa BWANA, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Haruni, kiinue mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako. “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Haruni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Siku zote hili litakuwa fungu la milele kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Haruni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa BWANA kutoka sadaka zao za amani.