Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 28:1-14

Kutoka 28:1-14 NENO

“Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Mshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima. Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haya ndio mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kizibau, kanzu, joho lililofumwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi. “Tengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi. Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kizibau. Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri. “Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine. Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu, na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kizibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za BWANA. Tengeneza vijalizo vya dhahabu na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.