Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 2:1-11

Esta 2:1-11 NENO

Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya, na alilokuwa ameamuru juu yake. Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Watafutwe wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme. Mfalme na awateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi wa mfalme, aliyekuwa msimamizi wa wanawake; na wapewe huduma zote za urembo. Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata. Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila la Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda. Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki. Agizo na amri ya mfalme ilipotangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa kwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake. Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya urembo na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake. Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wake na asili yake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza kufanya hivyo. Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.