Matendo 3:1-16
Matendo 3:1-16 NENO
Siku moja, Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali, yapata saa tisa alasiri. Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nitakachokupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu kwa yale yaliyomtukia. Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale Ukumbi wa Sulemani. Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea? Mungu wa Abrahamu na Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake. Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki, mkaomba mpewe yule muuaji. Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya. Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni jina la Yesu na imani kutoka kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama nyote mnavyoona.