Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 1:1-22

Matendo 1:1-22 NENO

Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyoyafanya na kufundisha tangu mwanzo, hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. Baada ya mateso yake, alijionesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu ufalme wa Mungu. Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?” Yesu akawaambia, “Sio wajibu wenu kujua nyakati au majira ambayo Baba ameyaweka kwa mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, Roho Mtakatifu akiwajilia juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na Yudea yote, na Samaria, na miisho ya dunia.” Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena. Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake mbinguni, ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao. Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni, atarudi tena jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini. Walipowasili mjini Yerusalemu, walienda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo na Andrea; Filipo na Tomaso; Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pia walikuwepo wanawake kadhaa, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake Yesu. Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao walikuwa watu wapatao mia moja na ishirini), akasema, “Ndugu zangu, ilibidi andiko litimie, ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda, aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu. Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.” (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu.) “Kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Zaburi, “ ‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’ Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiishi kati yetu, kuanzia ubatizo wa Yohana hadi siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”