Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 5:6-25

2 Samweli 5:6-25 NENO

Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi. Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.” Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani. Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu BWANA Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye. Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. Naye Daudi akafahamu kuwa BWANA amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake. Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake. Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai, kwa hiyo Daudi akamuuliza BWANA, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” BWANA akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu. Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua. Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai. Kwa hiyo Daudi akamuuliza BWANA, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa BWANA ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” Basi Daudi akafanya kama BWANA alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.