2 Samweli 13:1-14
2 Samweli 13:1-14 NENO
Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, dada yake Absalomu mwana wa Daudi, aliyekuwa mzuri wa sura. Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote. Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana. Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?” Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.” Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ” Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.” Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.” Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani mwa nduguye Amnoni, ndugu aliyekuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka. Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula. Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliye hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka. Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake. Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.” Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu. Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri.