2 Samweli 12:13-23
2 Samweli 12:13-23 NENO
Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya BWANA.” Nathani akamjibu, “BWANA amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za BWANA kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.” Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, BWANA akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao. Ilipotimia siku ya saba, yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.” Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.” Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya BWANA, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani mwake, akaomba wamwandalie chakula, naye akala. Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.” Akajibu, “Mtoto alipokuwa angali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? BWANA aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitaenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”