2 Wafalme 22:14-20
2 Wafalme 22:14-20 NENO
Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili. Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma. Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza BWANA, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za BWANA uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema BWANA. Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ” Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.


