1 Samweli 26:13-25
1 Samweli 26:13-25 NENO
Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama BWANA aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa BWANA. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?” Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama BWANA amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za BWANA! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa BWANA wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa BWANA. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.” Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.” Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. BWANA humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. BWANA alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa BWANA. Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa BWANA na kuniokoa kutoka taabu zote.” Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.” Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.