1 Samweli 23:14-29
1 Samweli 23:14-29 NENO
Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake. Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” Wote wawili wakafanya agano mbele za BWANA. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi. Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.” Sauli akajibu, “BWANA awabariki kwa kunifikiria. Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana. Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.” Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi. Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi. Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.