1 Samweli 13:1-14
1 Samweli 13:1-14 NENO
Sauli alikuwa na umri wa miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na mbili. Sauli alichagua watu elfu tatu kutoka Israeli; miongoni mwa hao, watu elfu mbili walikuwa naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli; nao watu elfu moja walikuwa na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao. Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!” Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, na sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali. Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita elfu tatu, waendesha magari ya vita elfu sita, na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki mwa Beth-Aveni. Waisraeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katika miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki. Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani hadi nchi ya Gadi na Gileadi. Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu. Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika. Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa. Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki. Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?” Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi, nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa BWANA.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.” Samweli akamwambia Sauli, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya BWANA Mungu wako aliyokupa. Kama ungetii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya BWANA.”