1 Samweli 1:7-20
1 Samweli 1:7-20 NENO
Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya BWANA, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula. Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?” Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la BWANA. Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba BWANA, akilia kwa uchungu. Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee BWANA wa majeshi, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa BWANA kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.” Alipokuwa anaendelea kumwomba BWANA, Eli alichunguza kinywa chake. Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa naye akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achilia mbali mvinyo wako.” Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa BWANA. Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa kutokana na uchungu mkuu na huzuni.” Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.” Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena. Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za BWANA na kisha wakarudi nyumbani mwao huko Rama. Elkana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye BWANA akamkumbuka. Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina Samweli, akisema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa BWANA.”