1 Wafalme 8:12-21
1 Wafalme 8:12-21 NENO
Ndipo Sulemani akasema, “BWANA alisema kwamba ataishi katika giza nene; naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.” Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. Kisha akasema: “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo na Jina langu liwe humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’ “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’ “BWANA ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu, na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile BWANA alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la BWANA alilofanya na baba zetu alipowatoa Misri.”