Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6

6
Solomoni Ajenga Hekalu
(2 Nyakati 3)
1 Katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, ambao ndio mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Bwana.
2Hekalu hilo Mfalme Solomoni alilojenga kwa ajili ya Bwana lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini,#6:2 Dhiraa 60 ni sawa na mita 27. upana wa dhiraa ishirini#6:2 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9. na kimo cha dhiraa thelathini#6:2 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5. kwenda juu. 3 Baraza ya mbele ya Hekalu ilienea dhiraa ishirini kulingana na upana wa Hekalu na kujitokeza dhiraa kumi mbele ya Hekalu. 4 Akatengeneza madirisha membamba yenye vidirisha vidogo vya juu katika Hekalu. 5 Akafanyiza vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote vikishikamana na kuta za Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. 6 Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano,#6:6 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25. ya kati ilikuwa dhiraa sita na ya tatu ilikuwa dhiraa saba.#6:6 Dhiraa saba ni sawa na mita 3.15. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
7Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika sauti yake katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
8 Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu, ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutokea hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu. 9Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mierezi. 10 Mfalme Solomoni akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mierezi.
11 Neno la Bwana likamjia Solomoni kusema: 12 “Kwa habari ya Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, kwa kupitia wewe nitatimiza ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. 13 Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”
14 Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha. 15 Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mierezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. 16 Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mierezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. 17 Ukumbi mkubwa uliokuwa mbele ya chumba hiki ndio ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini.#6:17 Dhiraa 40 ni sawa na mita 18. 18 Hekalu ndani ilikuwa ya mierezi iliyonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi, hakuna jiwe ambalo lilionekana.
19 Ndani ya Hekalu akatengeneza sehemu takatifu ya ndani, kwa ajili ya kuweka Sanduku la Agano la Bwana. 20 Sehemu takatifu ya ndani ilikuwa na upana, urefu na kimo cha dhiraa ishirini ndani kwa ndani. Akaifunika ndani kwa dhahabu safi, pia akaifunika madhabahu ya mierezi vivyo hivyo. 21 Solomoni akaifunika sehemu ya ndani ya Hekalu kwa dhahabu safi, naye akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande moja hadi ule mwingine mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, ambako palifunikwa kwa dhahabu. 22 Basi akafunika sehemu yote ya ndani kwa dhahabu. Pia akafunika madhabahu yale yaliyokuwa ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kwa dhahabu.
23Katika Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi#6:23 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5. kwenda juu. 24Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. 25Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, hivyo makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. 26Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. 27Aliwaweka makerubi hao ndani ya Patakatifu pa Patakatifu pa Hekalu, mabawa yake yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. 28Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
29Juu ya kuta zote zilizozunguka Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi zilizokatwa za makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua. 30Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.
31Kwa ingilio la Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza milango ya mbao za mzeituni, zikiwa na miimo na vizingiti vyenye umbo la pembe tano. 32Juu ya milango miwili ya mbao za mzeituni alinakshi makerubi, miti ya mitende pamoja na maua yaliyochanua na kufunika makerubi na miti ya mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. 33Kwa njia iyo hiyo akatengeneza miimo yenye pande nne ya miti ya mizeituni, kwa ajili ya ingilio la ukumbi mkubwa. 34Kulikuwa na milango miwili iliyoweza kukunjuka iliyotengenezwa kwa mbao za msunobari na kila mmoja ulikuwa na bawaba ambazo zingeuwezesha kujikunja kila kipande juu ya kingine. 35Akanakshi makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua juu yake na kufunika kwa dhahabu iliyonyooshwa vizuri juu ya michoro.
36Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa na safu moja ya boriti za mierezi zilizorembwa.
37Msingi wa Hekalu la Bwana uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa tano. 38Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Solomoni. Alilijenga kwa miaka saba.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 6: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha