1 Wakorintho Utangulizi
Utangulizi
Korintho ulikuwa mji uliojengwa pwani ya Mediterania (yaani Bahari Kuu). Mji huu ulistawi kwani ulikuwa kituo kikuu cha biashara. Ulikuwa koloni la Kirumi, ukiwavutia wakazi wa mataifa mbalimbali, wakiwemo Warumi, Wayunani na Wayahudi kutoka sehemu zilizoizunguka Bahari Kuu. Mchanganyiko huu wa wakazi ulisababisha kuharibika na kuzorota kwa maadili.
Paulo alianzisha kanisa mjini Korintho katika safari yake ya pili kueneza Injili, na akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Aliondoka Korintho akifuatana na Prisila na Akila kwenda Efeso, na kutoka huko alitembelea kanisa la Yerusalemu, na baadaye akarudi Antiokia. Paulo alipokea habari kutoka kwa nyumba ya Kloe kwamba kanisa lilikuwa limegawanyika. Paulo aliona ni muhimu awaandikie waraka huu ili kujibu matatizo mengi yaliyojitokeza. Aliposhughulikia matatizo haya moja kwa moja, Paulo alifafanua misingi ya mafundisho ya Kikristo kuhusu imani na maadili.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Kusudi
Kusahihisha makosa dhahiri katika kanisa la Korintho, na pia kuwaelimisha waumini jinsi ya kumtumikia Kristo katika jamii iliyokosa maadili.
Mahali
Efeso.
Tarehe
Mnamo 55 B.K.
Wahusika Wakuu
Paulo, Timotheo, nyumba ya Kloe, waumini wa Korintho.
Wazo Kuu
Umuhimu wa mwenendo wa Mkristo kufanana na Kristo.
Mambo Muhimu
Suluhu za matatizo mbalimbali kama: ugomvi kanisani, uzinzi, kushtakiana, mabishano juu ya ndoa, chakula kilichotolewa kwa sanamu, hali ya Paulo kuwa mtume, matumizi mabaya ya meza ya Bwana, ukweli kuhusu ufufuo, na mengine. Lazima mwenendo wa Mkristo ufanane na ule wa Kristo; kukosa kufanya hivyo ni kumwaibisha Kristo na kanisa lake.
Yaliyomo
Salamu za Paulo (1:1‑9)
Tatizo la mgawanyiko katika kanisa (1:10–4:21)
Tatizo la zinaa katika kanisa (5:1‑13)
Tatizo la kushtakiana mahakamani (6:1‑11)
Tatizo la uasherati (6:12‑20)
Tatizo kuhusu ndoa (7:1‑40)
Matatizo kuhusu uhuru binafsi (8:1–11:16)
Matatizo kuhusu meza ya Bwana na ibada (11:17–14:40)
Matatizo kuhusu ufufuo wa wafu (15:1‑58)
Mawaidha ya mwisho (16:1‑24).
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho Utangulizi: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.