Zaburi 107
107
Kitabu cha Tano
(Za 107–150)
Zaburi 107
Kumsifu Mungu kwa wema wake
1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema,
fadhili zake zadumu milele.
2 Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi,
wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,
3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,
kutoka mashariki na magharibi,
kutoka kaskazini na kusini.
4 Baadhi yao walitangatanga jangwani,
hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.
5 Walikuwa na njaa na kiu,
nafsi zao zikadhoofika.
6 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
7 Akawaongoza kwa njia iliyo sawa
hadi mji ambao wangeweza kuishi.
8 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,
na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.
10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu,
wafungwa wakiteseka katika minyororo,
11 kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu,
na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana.
12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu;
walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia.
13 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu
na akavunja minyororo yao.
15 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba
na kukata mapingo ya chuma.
17 Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao,
wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.
18 Wakachukia kabisa vyakula vyote,
wakakaribia malango ya mauti.
19 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
20 Akalituma neno lake na kuwaponya,
akawaokoa kutoka maangamizi yao.
21 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
22 Na watoe dhabihu za kushukuru,
na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.
23 Wengine walisafiri baharini kwa meli,
walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.
24 Waliziona kazi za Bwana,
matendo yake ya ajabu kilindini.
25 Kwa maana alisema na kuamsha tufani
iliyoinua mawimbi juu.
26 Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini;
katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.
27Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi,
ujanja wao ukafikia ukomo.
28Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawatoa kwenye taabu yao.
29 Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono,
mawimbi ya bahari yakatulia.
30 Walifurahi ilipokuwa shwari,
naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.
31 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu,
na wamsifu katika baraza la wazee.
33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa,
chemchemi za maji zinazotiririka kuwa ardhi yenye kiu,
34 nchi inayozaa ikawa ya chumvi isiyofaa,
kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.
35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji,
nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zinazotiririka;
36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo,
nao wakajenga mji wangeweza kuishi.
37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu,
nayo ikazaa matunda mengi,
38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana,
wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.
39 Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa
kwa kuonewa, maafa na huzuni.
40 Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu,
aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.
41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao,
na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.
42 Wanyofu wataona na kufurahi,
lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.
43 Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya,
na atafakari upendo mkuu wa Bwana.
Selectat acum:
Zaburi 107: NEN
Evidențiere
Copiază
Compară
Împărtășește
Dorești să ai evidențierile salvate pe toate dispozitivele? Înscrie-te sau conectează-te
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.